Serikali inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu hatima ya wanafunzi wa Gredi ya Sita, ambao wanatarajiwa kufanya mtihani wao wa kitaifa baadaye mwezi huu wa Novemba chini ya Mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).
Waziri wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu, jana Ijumaa alisema kuwa Rais William Ruto ndiye atatoa mwelekeo iwapo wanafunzi watajiunga na sekondari tangulizi au wataelekea Darasa la Saba kurejea katika mfumo wa 8-4-4.Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa mwezi Desemba.
“Kati ya masuala ambayo tunajikuna kichwa ni watahiniwa wa Gredi ya Sita ambao wanatarajiwa kujiunga na sekondari tangulizi. Nina hakika jopokazi lililoundwa kubaini ufaafu wa CBC litatoa ripoti ambayo itagusia suala hilo kwa Rais, baada ya muda wao wa miezi sita kutamatika,” akasema Bw Machogu.
“Mtihani wao unaanza Novemba 28 na tangazo rasmi litatolewa kabla ama wakati nikitoa matokeo ya mtihani huo. Rais atakuwa amefahamishwa kuhusu maoni ya Wakenya na kisha atatoa msimamo wa serikali,” alieleza.
Bw Machogu alikuwa akizungumza mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, jana Ijumaa aliposhuhudia jopokazi lililobuniwa na Rais Ruto kuhusu mageuzi katika sekta ya elimu, likipokea maoni ya wananchi.
Jopo hilo linaongozwa na Profesa Stephen Mbugua kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (CUEA).
Linajumuisha wasomi wengi na limekuwa likipokea maoni ya Wakenya kuhusu marekebisho ambayo yanastahili kukumbatiwa na serikali ili kuimarisha sekta ya elimu.
Kati ya masuala Wakenya wamekuwa wakitoa maoni yao ni kuhusu ufaafu wa CBC na gharama ya kuitekeleza, wanafunzi wa Gredi ya Sita kujiunga na sekondari tangulizi, na jinsi wazazi wanavyoweza kushirikishwa katika kuboresha elimu ya watoto wao.
Wazazi wamekuwa wakiishinikiza serikali kupitia Wizara ya Elimu itoe mwelekeo iwapo wanafunzi wa Gredi ya Sita watajiunga na shule za sekondari tangulizi au darasa la kawaida la saba; lengo likiwa wajiandae mapema kutimiza mahitaji yatakayoibuka.
Jopo hilo pia linatarajiwa kupokea maoni kuhusu kuimarishwa kwa taasisi za mafunzo na za kiufundi, vyuo vikuu na utafiti.
Chama cha Walimu wa Shule za Upili (KUPPET) kimeshauri serikali kuwa, wanafunzi wa Gredi ya Sita wanastahili kusonga mbele kujiunga na sekondari tangulizi katika shule za msingi wanakosomea kwa sasa, baada ya kufanya mtihani wao wa kitaifa mwezi huu.
“Baada ya mtihani, wanafunzi wanafaa kuingia Gredi ya Saba katika shule zao za sasa (za msingi),” alihoji Katibu wa Kaunti Robert Miano.
Baadhi ya wazazi nao wamekuwa wakidai kuwa watoto hao bado ni wadogo mno hivyo wanahitaji mwongozo wao kabla kuingilia masomo ya upili.
Wakati wa kikao cha jopokazi kupokea maoni ya umma, kilichoandaliwa katika ofisi za hazina ya ustawi wa maenebunge (CDF) mjini Nanyuki, wazazi walisema CBC ilitekelezwa kwa haraka na imeleta gharama kubwa sio kwao tu bali hata walimu ambao wanahitaji mafunzo mara kwa mara kuhusu utekelezaji wake.