Site icon The Black Board Kenya

CBC Yagubikwa na Utata huku Utekelazaji wake Ukiwa Gizani

Wazazi wanaotoa maoni mbele ya jopo kazi linalochunguza ufaafu wa mtaala wa Utendaji na Umilisi (CBC), wamependekeza mageuzi kadhaa kabla ya wanafunzi kujiunga na shule za sekondari ya chini.

Katika Kaunti ya Nyandarua, wazazi waliambia jopo lililoundwa na Rais William Ruto, kwamba watoto wao ni wachanga kuhudhuria sekondari ya chini katika shule za sekondari za mabweni.

Wazazi hao walisema kwamba wanataka sekondari ya chini inayoanzia Gredi 7 kuwa katika shule za msingi ili kuwezesha watoto wao kukomaa na kupashwa tohara kwanza.

“Mimi siko tayari kupeleka mtoto wangu katika shule ya sekondari ambako atatangamana na wanafunzi waliokomaa kama haitakuwa shule ya kutwa. Tulizoea kuwapasha watoto tohara kabla ya kujiunga na sekondari na ni wachanga sana kutahiriwa kwa wakati huu,” mzazi Steven Mucheru, aliambia jopo hilo.

Naibu Mwenyekiti wa chama cha walimu wakuu wa shule za sekondari (KESSHA) sekondari kaunti ya Nyandarua, Bw Peter Maina, alisema kuna uwezekano wa watoto hao kupata matatizo ya kisaikolojia kwa kudhulumiwa na wale wakubwa katika shule za sekondari.

Katika kaunti ya Kwale, wazazi waliambia jopokazi hilo kwamba mtaala huo ni ghali mno na utekelezaji wake unafaa kusimamishwa kwa kuwa tayari wanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi.

Bw Ali Abdalla, alisema kwamba mtaala huo unafaa kwa wazazi walio na uwezo wa kifedha lakini ni mzigo kwa wale maskini.

“CBC inaonekana kugubikwa na utata tangu mwanzo na hata wadau wanaohusika na utekelezaji wake wako gizani,” alisema.

Wakazi na wadau katika Kaunti ya Turkana nao walitaja ukosefu wa usalama na usawa kama changamoto kuu zinazokumba utekelezaji wake mtaala huo.

Mwenyekiti wa tawi la Turkana la chama cha kitaifa cha walimu Kenya, Bw Kenyaman Ariong’oa, aliambia jopokazi hilo linaloongozwa na Profesa Raphael Munavu, kwamba shule katika maeneo yanayokumbwa na ujangili hufungwa mara kwa mara huku wanafunzi wakiwa baadhi ya wanaouawa kwenye mashambulizi shuleni au vijijini.

Nacho chama cha Walimu wa Elimu Maalum Kenya (KUSNET), kililalamikia jinsi mtaala huo unavyotekelezwa kikisema walimu hawana mafunzo ya kutosha.Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw James Torome, alisema kwamba kama wazazi hawana mafunzo ya kutosha kutambua uwezo wa wanafunzi wachanga, basi, wanafunzi hao hawawezi kunufaika na mtaala huo mpya.

“CBC inahusu kutambua na kukuza uwezo au talanta, walimu wakishindwa kutambua talanta katika wanafunzi wa umri mdogo, basi mfumo huo hautawafaidi kamwe,” alisema.Bw Amos Karanja, ambaye ni afisa wa chama hicho, alisema kwamba ili mtaala huo uweze kufaulu, lazima kuwe na vifaa vya kutosha vya kufunza watoto walio na ulemavu ili talanta zao zitambuliwe mapema.

Share the story
Exit mobile version