Site icon The Black Board Kenya

KCSE: Mwalimu Mkuu Mbaroni Kwa Kusambaza Mtihani

Mwalimu mkuu wa Shule moja ya Upili Kaunti ya Machakos amekamatwa kwa kuchapisha mtandaoni mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne, KCSE unaoendelea.

Betta Mutuku wa shule ya ABC Kiseveni alitiwa mbaroni Jumanne, kwa kuchapisha mtihani wa Somo la Hesabu katika mtandao wa WhatsApp.

Maafisa kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), wakiongozwa na mkuu wa kitengo hicho Machakos, Rhodah Kanyi walimkamata mwalimu huyo akiwa shuleni na kumpeleka katika kituo cha polisi ili kuhojiwa zaidi.

Inasemekana mwalimu huyo alianza kuchapisha mtihani huo Jumatatu jioni, katika akaunti yake ya WhatsApp (status), ili watahiniwa waudurusu.

Somo la Hesabu limefanywa hii leo Jumanne.

Rununu ya mwalimu huyo ilitwaliwa na maafisa wa DCI, kwa minajili ya uchunguzi.

SOMA: Magoha Abamba Afisa Akisaidia Watahiniwa wa KCSE kwa Udaganyifu

Juma lililopita, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alikana kufuja kwa KCSE inayoendelea.

Waziri Magoha hata hivyo alionya kuwa wahusika wa udanganyifu katika zoezi hilo la mtihani watakaopatikana watachukuliwa hatua kisheria.

“Hakuna atakayesazwa, kuanzia watahiniwa, walimu, wasimamizi shuleni na katika vituo vya kusambaza mitihani. Tutawachukulia hatua kisheria,” alionya Prof Magoha.

Visa kadha vya udanganyifu katika KCSE inayoendelea hata hivyo vimeripotiwa, wahusika wakitiwa nguvuni.

Share the story
Exit mobile version