WABUNGE wameshinikiza serikali iongeze mgao wa fedha za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) wakisema wanahitaji pesa hizo kufadhili ujenzi wa madarasa zaidi katika shule za umma.
Shinikizo hizo zinatolewa huku ikisalia siku chache kabla wanafunzi kurudi shuleni Jumatatu ijayo, huku shule nyingi zikikumbwa na uhaba wa madarasa.
Mbunge wa Naivasha, Bi Jayne Kihara alisema fedha ambazo zimekuwa zikitolewa kwa NG-CDF hazitoshi kujenga madarasa mapya. “Fedha zinazotolewa zinatumika katika miradi iliyokuwa imepangwa kabla ya kutokea kwa janga la corona,” akasema Bi Kihara.
Mbunge huyo alisema shule nyingi za umma katika eneo lake zina zaidi ya wanafunzi 2,000 na zinahitaji madarasa zaidi kupunguza msongamano.
Katika mwaka huu wa matumizi ya fedha, Hazina Kuu ya Kitaifa imetenga jumla ya Sh41 bilioni kwa ajili ya hazina za NG-CDF katika maeneobunge yote 290.
Kila eneobunge hupokea mgawo wa Sh137 milioni kila mwaka.Mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale alisema itakuwa vigumu kwa wabunge kutekeleza wito wa Rais Uhuru Kenyatta aliyewataka washirikiane kuboresha miundomsingi shuleni, ikiwa hakuna pesa.
Mnamo Jumatatu, wabunge kutoka Kaunti ya Kiambu wakiongozwa na Mbunge wa Kiambu Mjini, Bw Jude Njomo, walilalamika kwamba serikali imetenga wabunge katika maandalizi ya kufungua shule wakati kungali kuna janga la corona.